By
bibikuku
|
PRESIDENT KAGAME OF RWANDA AND PRESIDENT KIKWETE OF TANZANIA IN A MEDIATION MEETING IN KAMPALA, UGANDA |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Alhamisi, Septemba 5, 2013, amekutana kwa faragha na Rais wa
Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame katika mazungumzo yaliyokwenda vizuri na
kuwaridhisha viongozi hao wawili wa nchi jirani.
Viongozi hao wamekutana kwa zaidi kidogo ya saa moja katika mkutano
uliofanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya
mji wa Kampala, Uganda.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Rais Kagame wamekubaliana
kuendelea kushirikiana katika kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria
uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao wawili wako nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi
Wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Maziwa Makuu – “International
Conference on the Great Lakes Region (ICGLR)” unaofanyika leo Hoteli ya
Munyonyo Commonwealth Resort.
Viongozi wengine ambao wanahudhuria Mkutano huo ni pamoja na Rais Yoweri
Museveni wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR na mwenyeji wa
Mkutano huo, Rais Silva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Joseph Kabila wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Mwenyekiti wa Kamisheni ya
Umoja wa Afrika (AU).
Rais Kikwete na ujumbe wake amewasili Kampala asubuhi ya leo akitokea
mjini Dodoma ambako aliwasili jana jioni kwa ajili ya hafla ya
kuwaapisha Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuuu wawili
iliyofanyika Ikulu Ndogo, Dodoma.
Rais Kikwete aliwasili Dodoma akitokea Mwanza ambako alihudhuria mazishi
ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania
(EAGT) Askofu Mkuu Dkt. Moses Samwel Kulola yaliyofanyika kwenye Kanisa
la Bugando Calvary Temple, mjini Mwanza.
No comments:
Post a Comment